Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Mashhad, Farid Ishaq, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini, katika jopo la kielimu la Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Teolojia ya Muqāwama, lililofanyika katika Kitivo cha Sayansi cha Chuo Kikuu cha Ferdowsi cha Mashhad, alieleza uhusiano kati ya teolojia na kitendo cha kimapinduzi. Katika muktadha huo, alilinganisha kauli mbili: “al-sultān dhillullāh fīl-arḍh” na “likulli fir‘awn Mūsā” (kila Firauni ana Musa wake), na akafafanua nafasi ya lugha ya dini ya kuleta ukombozi katika mapambano dhidi ya Apartheid nchini Afrika Kusini.
Katika ufafanuzi wa mada ya hotuba yake alisema: Kuanzia miongo ya miaka ya 1970 na 1980, mkusanyiko wa misemo na dhana za kimapinduzi za Kiislamu—zilizotokana na mageuzi ya kifikra katika ulimwengu wa Kiislamu na tajriba ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran — vilianza kuingia taratibu katika miundo ya harakati za kupinga Apartheid na za ukombozi miongoni mwa Waislamu wa Afrika Kusini. Dhana kama mustadh‘afūn fīl-arḍh (waliodhulumiwa duniani), istikbār na mustakbirīn dhidi ya mustadh‘afīn, kaulimbiu ya “Si Mashariki wala Magharibi” yenye msisitizo wa tauhidi ya Kimungu, pamoja na kauli “likulli fir‘awna Mūsā”, zilitumika kama zana madhubuti za lugha zilizofungua upeo mpya wa kuisoma upya Qur’ani na kuhamasisha kitendo cha kijamii.
Ishaq aliongeza kuwa: Sehemu ya istilahi hizi mwanzoni ilijitokeza katika sura ya kaulimbiu za maandamano, lakini kwa wakati huo huo zilifanya kazi kama njia fupi za kimaana, ambazo kwa kuzielekeza upya kwa busara dhana zilizopo za Qur’ani, zilizisukuma kuelekea usomaji wa kimapinduzi na wa kuleta ukombozi. Mchakato huu ulikuwa na mchango mkubwa katika kuibuka kwa teolojia ya Kiislamu ya ukombozi nchini Afrika Kusini, na pia katika baadhi ya maeneo duniani baada ya mwaka 1979; na dhana nyingi kati ya hizi bado zina nafasi muhimu katika hotuba ya leo ya teolojia ya Kiislamu ya ukombozi.
Mhadhiri huyo aliendelea kwa kuzingatia kaulimbiu “likulli fir‘awna Mūsā”, akiichambua kwa kuilinganisha na hekima iliyoenea zaidi katika mapokezi ya Kisunni, yaani “al-sultān dhillullāh fīl-arḍ”. Alieleza kuwa: Ingawa kauli ya pili imenukuliwa katika vyanzo vya Hadithi kwa viwango tofauti vya uthibitisho na imeenea katika jamii nyingi za Kisunni, kwa vitendo inaweza kuishia kutoa uhalali wa kidini kwenye tawala dhalimu na mamlaka zinazotawala kwa nguvu.
Kwa upande mwingine, alisema: Kaulimbiu “likulli fir‘awna Mūsā”, ambayo ilipata umaarufu mkubwa kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 nchini Iran, licha ya kuwa na uzito mdogo wa kiwasilishaji katika mapokeo, iliweza kuchochea fikra, matumaini na azma ya Waislamu waliokuwa wakishiriki katika mapambano ya ukombozi ya Afrika Kusini, na ikageuka kuwa injini ya kimaana ya muqāwama.
Alisisitiza kuwa: Ufanisi wa kaulimbiu hii hauko katika uthibitisho wake wa kihistoria, bali uko katika uwezo wake wa kuleta ukombozi na wa kuhamasisha; uwezo unaoipeleka teolojia kutoka kiwango cha tafsiri ya maandishi hadi katika uwanja wa kitendo cha kijamii, na kuifanya lugha ya dini kuwa chombo cha kudai haki, kusimama dhidi ya dhulma, na kukataa utawala wa mabavu.
Maoni yako